Free Web Hosting by Netfirms
Web Hosting by Netfirms | Free Domain Names by Netfirms


Ukurasa wa mbele
Gazeti la injili
Nyimbo za Munishi
Soma barua Yahoo
Soma barua Hotmail
Tuma SMS duniani
Sema nami
Sikiliza waongo

Twende kanisani

Gazeti INJILI http://munishi.netfirms.com
E-mail: munishifaustin@yahoo.com
Or fmunishi@hotmail.com

Maelfu wamzika Lianda


Marehemu Mchungaji Lianda Nakuru imezipokea habari za kifo chake kwa mshituko .

Aliyekuwa Mchungaji mwanzilishi wa kanisa la Assemblies of God Nakuru ameaga dunia. Mchungaji Lianda alifariki tarehe 12-6-2002 katika hospitali ya Agha Khan Nairobi. Madaktari walisema kilichosababisha kifo chake ni kansa. Kansa iliharibu kifuko cha nyongo, na kusababisha nyongo kutapakaa mwili mzima. Marehemu alikuwa na shida kubwa ya kujikuna mwili mzima, na mara nyingine mwili wake uligeuka kuwa rangi ya njano. Ni wakati madaktari walipomfanyia upasuaji ili kujaribu kuziba kifuko cha nyongo, ndipo walipogundua kwamba kansa ilikuwa imeharibu sehemu kubwa ya mwili wa mchungaji. Walifanya waliyoweza kuyafanya, na mengine walimwachia Mungu. Hata madaktari walishangaa kwamba mchungaji aliwezaje kuishi wakati sehemu za maini, figo, zilikuwa zimeharibiwa kiasi hicho. Mungu alipoamua kuichukua Roho ya Mchungaji, jamii na kanisa walisema,: "Ni yeye aliyetupatia Mchungaji LIANDA, na ni yeye ameamua kumchukua. Jina lake litukuzwe kwa yote."

Tarehe 21-6-2002. Maelfu ya Wakristo na wasiyo wakristo walimiminika katika Makaburi ya mji wa Nakuru kutoa heshima zao za mwisho kwa mchungaji Lianda. Wengi walitoka mbali kama Tanzania Uganda, Nairobi na wengine kutoka katika vitongoji vyote vya Nakuru. Wachungaji wa makanisa karibu yote Nakuru walijiwakilisha wenyewe kumuaga Mchungaji mwenzi wao. Baba na mama wa marehemu pia walionekana wakiwa na huzuni kubwa ya kumpoteza kijana wao. Ndugu jamaa na marafiki wakiongozwa na dada mkubwa wa marehemu Glady na mume wake John Dougas kutoka Arusha Tanzania, pia walikuwepo kutoa heshima zao za mwisho. Askofu Geofrey Buliba wa kanisa loa CBC pia alikuwepo kumuaga kwa mara ya mwisho mchungaji na rafiki wa karibu marehemu Lianda. Pia waimbaji wa injili hawakuachwa mbali kwani walijitokeza kwa makumi yao kuimba na kupamba kile wengine walichokuwa wakikiita sherehe. Mimi sikuona sababu ya kuita maziko ya mtumishi wa Mungu shererhe, kwani biblia inaturuhusu kuomboleza na wale waombolezao. Pia Neno la Mungu linaturuhusu kuwalilia wale tuwapendao hata kama tuna hakika kwamba hawakwenda pabaya. Niseme tu kwamba kila mtu alikuwepo kufanya kile moyo wake ulichomtuma kufanya siku hiyo. Walisheherekea walifanya hivyo, na walioomboleza walifanya hivyo kwa nguvu zao zote.

Wote walikuwepo kutoa heshima zao za mwisho.Kutoka kushoto ni watoto wawili wa Lianda pamoja na mama yao, wakifuatia na shemeji yaoaliyemuoa mmoja wa watoto wa Lianda na dada yake.

Kama wafu waliolala makaburi ya Nakuru wangekuwa wanasema, basi wangesema tarehe 21-6-2002. Walikanyagwa, walikaliwa, na isitoshe walipigiwa kelele na vyombo vya kupazia sauti. Nilipofika katika makaburi ya Nakuru mjini, nilingojea kwa hamu kusikia malalamiko kutoka kwa wale ambao hapo ni mahali pao pa kupumzika baada ya safari yao kumalizika duniani, lakini sikusikia. Umati mkubwa uliofika hapo siyo kwamba uliyakanyaga makaburi tu, wengine waliyakalia baada ya kuchoka kusimama. Watoto nao waliyachukua maua juu ya makaburi hayo na kuanza kuyachezea. Ninavyomfahamu Marehemu Lianda, sidhani kama angependa iwe hivyo.

Aliamini kwamba Yesu mwenyewe mazishi yake yalifanywa na mtu mmoja aliyeomba mwili wake na kuulaza kwenye kaburi bila maonyesho mengi. Kama huko waliko huwa wanasemezana, basi siku hiyo walikuwa wakiulizana nani huyu aliyeletwa hapa na umati mkubwa namna hii hata kutuharibia starehe yetu ya usingizi? Alikuwa siyo mwingine ila ni Mchungaji Lianda wa kanisa la Kenya Assemblies of God. Umati uliojumuisha wachungaji na washirika wa makanisa yote Nakuru, uliifanya sehemu hiyo ambayo kwa kawaida ni kimya na tulivu kuwa uwanja wa mkutano wa Injili. Tangu saa nne asubuhi mpaka saa kumi na moja jioni makaburini Nakuru ilikuwa na pilika-pilika na patashika ya nguo kuchanika.


Tumsaidie Mke wa Mchungaji Lianda


Marehemu Mchungaji Lianda akiwa na Mke wake.

Majukumu yote ya Kanisa na jamii ya marehemu yako kwa mke wake sasa. Kuna watoto wanaosoma, Nyumba ya kujenga na kanisa la kuchunga. Mara nyingi mchungaji akiondoka washirika huwa na tabia ya kumsahau mke wa mchungaji. Hii ni kutokana na ukweli kwamba aliyekuwa akionekana sana ni Mchungaji na siyo mke wake. Wanasahau kwamba kila walipokuwa wanamuona mchungaji akiwa amevalia vizuri huyo alikuwa mke wake ndani ya mchungaji.Hata Injili aliyoihubiri kwa ufasaha, asingefanya hivyo kama siyo mke wake kusimama naye katika maombi. Kwa hiyo kanisa litakosea sana kama litamwacha mama mchungaji ateseke na jamii, kwa sababu tu mchungaji ametangulia kupumzika. Ni jukumu letu kama kanisa kumtunza mke wa mchungaji hata zaidi ya wakati mchungaji mwenyewe akiwepo. Wakati umefika wa kanisa kuamka na kufanya yale lililotarajiwa kuyafanya. Nayo ni kuwatunza wajane wote hata kama siyo wake wa wachungaji. Badala ya kutumia vibaya pesa za kanisa kununulia magari ya kifahari, ni vizuri zitumike katika kuwahudumia wenye mahitaji kanisani ambao ni wengi. Ukiyaaangalia magari ya kifahari yanayoendeshwa na wachungaji wa Kiafrika, utashangaa kwani hata huko Amerika wachungaji hawathubutu kutembelea magari ninayoyaona na waafrika wenzetu wachungaji. Tunachosema hapa siyo wachungaji watembelee pikipiki, ila kama watanunua magari yawe ni kwa ajili ya kuisaidia huduma yao ya kuhubiri, na siyo kujionyesha kama wanasiasa wafanyavyo.

Lianda Pumzika Inatosha


Marehemu Mchungaji Lianda kushoto, na Bishop Mark Kariuki kulia Ambaye marehemu alimlea kiroho kabla ya kutoka na kuwa mpinzani wake NO. 1

Mchungaji Lianda atafananishwa na Paulo, Mark Kariuki ni Timotheo wake. Alimfundisha Mark Kariuki neno la Mungu alipokuwa mwalimu wa shule ya msingi kuanzia mwaka 1982 mpaka mwaka 1983 wakati Mark Kariuki alipoamua kuacha kazi yake aliyoisomea na kuwa mhubiri bila kwenda shule ya biblia. Alipoamua kutoka KAG na kuanzisha kanisa la ukombozi Nakuru mchungaji lianda hakuyaamini macho na masikio yake. Kama kuna mtu aliyekudangaya kwamba hakuna ukabila makanisani, alikosea. Mark Kariuki alihama na wakikuyu karibu wote kutoka kwa Lianda, jambo lililoanzisha vita baridi kati yao. Mji wa Nakuru kuanzia watoto hata wazee wanajua kwamba uhusiano kati ya hawa watumishi wa Mungu wawili haukua mzuri. Ni kweli kwamba walitembeleana na kujaribu juu chini kutokuonyesha uhasama kati yao. Lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba vita vya chini kwa chini vilikuwa vikiendelea kati yao. Hasa baada ya Mchungaji Mark Kariuki kununua uwanja uliopakana kabisa na mahali kanisa la KAG lilipo. Siku ya Jumapili ungepitia karibu na mahali hapo, ungeshindwa kujua kama utamsikiliza nani. Vyombo vya kupazia sauti vya hali ya juu vilitumika pande zote. Lakini ungelipitia hapo usingeshindwa kujua nani aliyelemewa. Aliyekuwa na vyombo vya nguvu zaidi kutoka Marekani ndiye anayesikika zaidi. Isitoshe ibada zinaendeshwa kama mashindano. Wengine waliuita usumbufu na siyo mahubiri kama wahusika walivyotutaka tuamini.


Danstan Maboya Kushoto na Moses Kulola kulia Maboya alilelewa kiroho chini ya Kulola, lakini sasa ni maadui wakubwa. Kulola humsuta Maboya madhabauni.

Inasikitisha kuona kwamba shetani anatumia mbinu hiyo ya ushindani kati ya wale wanaojiita watumishi wa Mungu. Mtu anaweza kufikiri kwamba hali hiyo iko Nakuru pekee. Hapana ni kila mahali.Tanzania Askofu Kulola na Dastan Maboya hawakai meza moja. Kila mmoja anamwita mwenziwe majina.


Wilfred Lai wa kwanza kushoto, na mpinzani wake James Ng'ang'a Wa tatu kushoto ni Mchungaji Mwarandu akifuatiwa na mpinzani wake mkali Pius Muiru.

Nairobi Mchungaji Mwarandu na PIUS MUIRU ni kama paka na panya. Mombasa Wilfred Lai na Pastor James Maina Ng'ang'a huchongoana kwenye mahubiri. Kila mmoja hudai kwamba mwingine amemchukulia kondoo wake. Swali la kujiuliza ni je! Nani alimwaga damu yake kwa ajili ya kondoo? Yesu ndiye aliyefanya hivyo, kwa hiyo kondoo ni mali yake.

Bishop Mark Kariuki alisema:

" Majirani hawakosi kugombana, na wakati mwingine kupigana." Wakati Mchungaji Lianda aliponiita, kwanza nilifikiri kwamba kondoo wangu wameruka fensi na kuingia kwake." Aliponiambia mambo kuhusu nyumba, sikumjibu hapo ila nilimwambia nitakwenda nifikiri." Sikuweza kumjibu wakati wa uhai wake, naona nililete hapa kwenu sasa." Ilihusu nyumba yake, na ninaona ni vyema tuchange pesa ili tuanze kuijenga nyumba yake ili jamii yake isifukuzwe kwenye nyumba."

Baadhi ya wachungaji hawakufurahia matamshi ya Askofu huyo. Wengi waliona kama anamdhalilisha marehemu. Lakini wengine walisema hapo ndipo palipofaa kuliweka wazi jambo hilo. au wewe unasemaje?

Kama kipimo cha uchungaji mwema ni magari ya fahari na nyumba kubwa, basi wachungaji wengi Nakuru wamempita Lianda kwa mbali. Kwenye mazishi yake askofu Mark Kariuki alisikika akisema kwamba marehemu aliwahi kumwita na kumweleza hitaji lake la nyumba. Askofu huyo aliwataka waombolezaji wachange ili kusaidia ujenzi wa nyumba hiyo. Watu waliingiwa na huzuni na kutoa pesa hapo kwa hapo ambazo idadi yake haikutangazwa. Wengi walisikika wakilalamika kwamba wachungaji waliyatumia mazishi ya Lianda kuonyesha umaarufu wao wa kuhubiri. Pengine walikuwa sawa. Tangu saa nne asubuhi ilikuwa ni mahubiri tuuu mpaka saa kumi na moja jioni ndipo mwili wa marehemu ulipowekwa mahali pa kupumzika.


Marehemu Lianda na jamii yake

Tofauti na wachungaji wengine ambao hutumia pesa za kanisa kujitajirisha kibinafsi, Lianda alikuwa akiishi katika nyumba ya kupangisha iliyoko karibu sana na kanisa alilokuwa akilisimamia. Alipenda sana kuwa karibu na kanisa, ndio maana alikataa kuhamia milimani ambako uongozi wa kanisa ulimtaka aishi huko. "Milimani ndio mtaa wa watu wazito." Lianda alishikilia msimamo wake kwamba Yesu amemuokoa na kumfanya mzito, na ahitaji gari kubwa na nyumba milimani ili kumuongezea uzito ambao tayari alikuwa nao. Mchungaji Lianda aliishi maisha ya kawaida kama mtumishi wa Mungu. Hakujitakia makuu. Usingeweza kumtofautisha na washirika wa kanisa lake, kwani aliishi kama wengi wao. Ni ukweli usiopingika kwamba wachungaji wengine huwezi hata kujaribu kuwalinganisha na washirika wao. Wanaendesha magari ya kifahari kama yaendeshwayo na wauza madawa ya kulevya. Washirika ambao ndio watoaji wa sadaka, wengi wao hawana hata baiskeli. Na wale waliobahatika kuwa na mali kidogo, hali yao inazidi kudidimia wakati mchungaji na jamii yake wanabadili magari kama nguo. Kwa Marehemu Lianda hal;i ilikuwa tofauti kabisa. Aliamini kwamba utajiri wa kanisa ni mali ya jumuia husika, na siyo mali yake binafsi. Hakuwahi kulipa mamilioni kuwa na kipindi katika TV wakati washirika hawana kituo cha afya na shule kwa ajili ya watoto wao. Aliamini kwamba vipindi hivyo hutumika kumwinua mtu mmoja na siyo kujenga mwili wa Kristo ambao ndilo KANISA.

Ameandika Faustin Munishi.
Mwinjilisti na mwimbaji wa nyimbo za injili. E-Mail fmunishi@hotmail.com
WEB SITE http://munishi.netfirms.com

 
| http://munishi.netfirms.com |
 
<<Back  |  Home |  Gazeti La Injili | Injili2 | Nyimbo Za Munishi | Next >>